Safari: Moyo na Mwenzake 01
Ilikuwa ni siku yake ya furaha. Taratibu alijongea na gauni lake ukumbini watu wote walimshangaa huku wakinong’onezana jinsi alivyopendeza, kwa aibu alitazama pande zote kwa tabasamu akiangalia ndugu, jamaa na marafiki waliohudhuria kwenye sherehe hiyo ya harusi kati yake na Maliki. Wimbo wa msanii Paul Clement; “Amefanya Mungu” ulikuwa unaburudisha mioyo ya wageni wote waalikwa.
“Mabibi na Mabwana namkaribisha kwenu Bibi harusi wetu Linda au kwasasa tunaweza kumwita Mrs. Maliki” Mshereshaji alisema kwa mbwembwe huku watu wote wakimsindikiza kwa makofi na vigerere huku wakiimba pamoja naye wimbo huo;
Je ni nani angeweza
kututoa chini mavumbini
maana kila mtu alitukataa
ila Mungu akatukumbatia.
Je ni nani angeweza
kutuinua kutuweka juu
Maana kila mtu alitukataa
Ila Mungu akatuinu...
Wanasema ukiwa unakata roho na kuiacha dunia maisha yako yote huwa yanapita kwenye macho yako lakini sio kwa Linda, hakutaka kusuburi hadi afikie kifo ndio ayaone yote hayo. Akiwa kwenye kilele cha furaha siku yake ya harusi kwenye zulia jekundu urefuu kadha kumfikia mume wake kipenzi mbele ya ukumbi kumbukumbu zilizochagizwa na wimbo huo zilimrudisha hadi kipindi anamaliza kidato cha nne kwenye shule ya sekondari Jangwani.
Ilikuwa ni siku ya mahafali yake ya kidato cha nne baada ya kusongoka kwa miaka minne hatimaye sasa naye alikuwa anamaliza elimu ya sekondari. Linda alikuwa ni mtoto wa pili kuzaliwa, wa kwanza akiwa dada yake kipenzi Rebeka na aliyemfwata ni kitinda mimba wao Emmanuel. Wazazi wao walijitahidi kuwalea kwenye maadili ya kidini na kijamii. Baba yake Linda alikuwa anafahamika sana mtaani kama mzee wa yanga kwasababu ya mapenzi yake kwa timu hiyo.
Ilikuwa ni jambo la kawaida katika familia yao siku mtu atakapo hitimu masomo kujumuika na kusheherekea naye pamoja. Siku hiyo walifanyia hapo hapo shuleni wakatafuta sehemu na kujibanza na kuanza kusherekea. Wanafunzi wengine pia walifanya hivyo. Walikata keki, wakapiga picha na kula. Watu wote kwenye familia walihudhuria pamoja na majirani wachache kasoro baba kwasababu alikuwa kazini.
Linda alikuwa ni msichana mwenye hisia sana. Pamoja na kusoma na wenzake kwa miaka yote minne hakutegemea kama ingekuwa vigumu kuagana kwa namna hiyo. Shule haikuwa ngumu sana kwake kwani alijitahidi kusoma na kushiriki kwenye shughuli mbalimbali lakini wazo la kumaliza shule lilikuwa jipya kwake ingawa alifurahi lakini pia alikuwa na huzuni. Rafiki yake kipenzi Janeth alimfuata baadaye baada ya mahafali kuisha na familia za wahitimu kuanza kutawanyika.
“Yaani siwezi amini ndo imeisha hivyo” alisema Janeth kwashauku huku akimkumbatia mwenzie na kumbana kwa nguvu.
“Hahah Jane, bado sana” alijibu Linda huku akijitoa kwenye mbano huo.
“Bado!, bado nini?”
“Kidato cha sita, chuo!”
“Hee! We unaenda form six”
“Ndio, kwani we huendi?”
“Aku! Mimi nishamwambia mama matokeo yakitoka naenda chuo moja kwa moja, mambo ya kuanza kuvaa sale tena kama watoto sitaki”
“Mhhh! Kumaliza tu siku moja unaita wenzio watoto?”
“Ndio! Hebu tuachane na hayo, vipi Amosi amekuja?”
Amosi alikuwa ni rafiki yake Linda ambaye alikutana nae kanisani, yeye alikuwa sio mwanafunzi bali anafanya kazi kwenye kampuni moja ya wahindi. Amosi alikuwa mkubwa kidogo kwa Linda lakini hilo halikuwa shida kwa Linda kwani alimpenda Amosi jinsi alivyo na umri ulikuwa sio kikwazo kwake hata hivyo hawakupishana sana.
“Aliniambia akipata nafasi atakuja lakini naona kashindwa maana anafanya kazi kwa Wahindi halafu si unajua wahindi walivyo…. Mmh” alisema Linda akiwa kama mwenye kukatishwa tamaa kwasababu Amosi hakutokea.
“Usijali mwaya”
“Mimi nipo sawa” alisema Linda huku akimkumbatia tena. Mara Janeth alikuja kuitwa na ndugu yake kuwa wanaondoka, wakaagana na kila mtu kurejea makwao.
Alipofika nyumbani hakutaka kupoteza mda alichukua Kitochi chake na kumtumia ujumbe Amosi. Alivyoona kimya akatuma tena. Na tena, na tena. Akachoka akaamua kupiga kabisa. Simu ilikuwa inaaita tu hadi ikakata. Akapiga tena, pia haikupokelewa. Akakasirika atupa simu kitandani akaenda kuoga. Alivyorejea pia kulikuwa hakuna kitu, hata ujumbe wowote. Ghafla akagongewa na mama yake huku akimwita.
“Abeeee” aliitika.
“Una mgeni wako”
Alishangaa! ‘Mgeni muda huu’“Nakuja” alijibu.
Haraka alijifuta maji na kuvaa nguo kisha akatoka. Alivyofika sebuleni alimkuta Amosi ameketi kwenye kochi akimsubiria. Alishtuka sana, kwani ilikuwa ndio mara ya kwanza kwa yeye kufika na kuingia nyumbani kwao. Siku zote alikuwa akimficha na walikutana mafichoni lakini leo ujasiri gani ulimuingia na kufika hadi nyumbani, tena ndani. Haraka haraka akamuinua na kutoka nae nje.
“Wewe Amosi, unafanya nini?” alifoka Linda baada ya kumtoa mbali kidogo na nyumbani.
“Nini shida kwani?”
“Nini shida? Pale ni nyumbani na nilishakuambia kuhusu nyumbani kwetu” aliongea kama akiwa ananong’neza.
“Mbona hamna shida yoyote na mama yako kanikaribisha vizuri” Amosi pia alijibu kwa mtindo ule ule.
“Basi tu umekuta tu leo kila mtu yupo vizuri. Je Baba angekukuta?”
“Mbona nimesalimiana naye!”
“Heee!”
“Eeeh! Tena yeye ndo kaniambia niingie ndani”
“We Amosi wewe!”
Linda alibaki akishangaa kichwani akifikiria ‘Mbona ghafla’ huku akimwangalia Amosi ambaye alionekana hana wasiwasi hata kidogo. Amosi alimshika mabega na kumuweka usawa wake na jinsi alivyokuwa mrefu akamshika kidevu na kumpandisha sura amtazame. Ni kama alikuwa akishangaa bendera kwenye mlingoti.
Amosi alitabasamu.
“Linda tatizo lako una hofu sana” alimwambia kwa upole.
“Sio kwamba nina hofu Amosi ni vile…”
“Shhh leo sitaki tugombane. Nimekuletea zawadi, hongera kwa kumaliza kidato cha nne Mpenzi” Amosi akanyoosha mkono akamkabidhi mfuko ambao ndani ulikuwa na boksi lililofungwa.
“Nini hii?”
“Mimi sijui… Labda ni bomu!” alimtania.
Linda akamkumbatia kwa nguvu na haraka “Basi tulipuke wote”
Taratibu akajivua kisha akakumbuka!
“Ulikuwa wapi? Mda wote nakupigia simu yako inaiita tu hadi inakata” akampiga kibao.
“Aaah! Kuhusu hilo, simu yangu nimesahau ofisini mezani wakati natoka. Sasa nipo njiani nataka nikutumie ujumbe tukutane tunapokutanaga Heee! Kumbe simu sina na ofisini siwezi rudi. Nitafanyaje wakati kwenu napajua. Nilijua tu utawaka kuhusu hili la kuja kwenu lakini nimejitoa mwanga na kila kitu kimeenda sawa”
“Sawa! Labda kwa upande wako” Linda alisema kwa unyonge kwa sauti ya kudeka.
“Usijali kipenzi kila kitu kipo sawa!”
Linda alifurahi sana kumwona Amosi usiku huo, kwani Amosi alijua kumpatia Linda. Alimjua kwa kila namna na Linda alijiona wa pekee na alifurahi kila alipokuwa nae karibu. Baada ya kuachana mahali hapo Linda taratibu alirudi nyumbani na alipofungua tu mlango wa sebuleni alikutana na jopo linamsubiria wote wakimkodelea macho; Mama, Baba, Dada yake Rebeka na Emma akiwa anachekacheka tu.
Ahsante kwa kusoma hadithi hii, ni mwanzo mzuri hivyo usikose kusoma mwendelezo wake.Unaweza changia juhudi hizi tunazozifanya kwa maoni, ushauri na utaalamu.