Safari: Moyo na Mwenzake 08
Pamoja na mawazo yote hayo, lilikuwa ni jambo moja kujua tatizo na jambo lingine kabisa kufanya au kuchukua uamuzi unaofaa. Linda hakuwa amefikiria kwamba labda kuna watu ndio wamemfanyia hivyo hata baada ya kuzunguka sana kwenye makanisa ndani ya miezi miwili bado mawazo yake hayajatua huko.
Siku akiwa amedhohofu sana kwenye kituo cha daladala akiwa amekaa yeye na mama yake wakisubiria daladala alikuja mtu kumwongelesha. Ilikuwa ni sauti aliyoifahamu ila kwasababu alikuwa amechoka sana hakuweza hata kujibu alichoongleshwa. Alikua amejifunika kichwa na kujizungushia mtandio kama alikuwepo sehemu yenye baridi. Mda wote alisikia maumivu, alihisi kama kuna kitu kinakwangua kwenye mapafu yake.
“Dada Linda Mambo?” alisema yule mtu. Sauti yake ilikuwa tulivu na ya upole.
“P...o..a” Linda alijibu kwa shida.
“Mbona umejikunyata hivyo nini shida?”
Linda hakuwa na nguvu za kujibu lakini alizidi kuifikiria sauti ya yule mtu; ‘Nani huyu ananiongelesha mbona kama namjua’ aliwaza Linda. Hakumjibu kitu. Mama yake aliingilia na kuanza kumwelezea mtu huyo. Kulikuwa hamna aibu kuzungumzia jambo hilo, Mama Linda aliamini mtu yoyote labda angejua jinsi ya kuwasaidia au kuwaelekeza sehemu yoyote ambayo wangeweza kupata msaada hata wa kimiujiza ili binti yake aweze kupona.
Linda hakusikiliza maongezi yao ila alizidi kufikiria ni nani hadi kwamba mama anamwambia mambo yote hayo kuhusu yeye wakiwa kwenye kituo cha daladala. Hakuweza kufanya kitu kwani alikuwa hana hata nguvu ya kujibizana na mtu. Baadae walipofika nyumbani na kupumzika kidogo Linda alipata nguvu za kumuuliza mama yake yule aliyekuwa akiwaongelesha kituoni alikuwa ni nani.
“Yaani hujasikia chochote, kijana wa watu amekuja pale amejitambulisha na ukaongea nae hukuweza kumtambua bado?” alisema Mama Linda.
“Hapana nilikuwa nasikia sauti tu;”
“Alisema anaitwa Joshua. Alikuwa ni rafiki wa karibu wa Amosi”
“Joshua!” Linda alisema kwa kushangaa huku akiwazua ndio maana alikuwa akiitambua ile sauti.
“Alitamani atusindikize hadi nyumbani sema alikuwa na haraka. Amesema atakuja kesho kukuona”
Linda aliamka alipokuwa amekaa na taratibu akajikongoja kuelekea chumbani kwake.
Mawazo ya Linda hayakuwa kwa Joshua tena alishatambua ni nani aliyekuwa anamuongelesha hilo lilikuwa sio la maana tena. Kilichokuwa cha maana sasa ni hatima yake ya masomo. Mipango yake yote ilivurugika na taratibu akaanza kulia kwa sauti ya chini. Alilia kwa uchungu akitafakari yanayomkuta au ndio mwisho wake ulikuwa unakuja kidogo kidogo?.
“Ni heri nife nijue moja kuliko kuteseka kwa namna hii. Mambo yote haya yana maana gani?” alisema kwa uchungu akiendelea kulia hadi akapitiwa na usingizi.
Kesho yake kama Joshua alivyoahidi alifika nyumbani kwa kina Linda. Mama Linda alimpokea na kumkaribisha ndani. Linda alikuwa chumbani kwake amejifungia kama kawaida yake, mama yake alikuja kumgongea na kumjulisha kuwa ana mgeni. Ili kutokujivuta sana mama yake alimharakisha, alimsaidia kujiweka vizuri kisha akamleta hadi sebuleni. Joshua alipomuona Linda alisimama na kumpokea kisha akaketi naye kochi moja.
“Mimi nitawaacha jamani nikaendelee na kazi nyingine” alisema Mama Linda.
“Hamna shida mama, we endelea tu” alijibu Joshua.
Baada ya mama kuondoka ukimya ulitawala kidogo. Joshua hakusema kitu wala Linda hakusema kitu. Joshua alikuwa akimtazama Linda kichwani akifikiria kitu. Linda naye akaamua avunje ukimya.
“Samahani… jana nilishindwa kukutambua kaka yangu” alisema Linda.
“Usijali… mama alinielezea kuhusu hali yako” alijibu Joshua.
“Imekuwa mda sasa… tulipoteana. Maisha yanaendaje?” aliuliza Linda.
“Tunamshukuru Mungu, Kila siku ni siku mpya ameifanya.” alisema Joshua kisha akaendelea “Vipi wewe masomo yanaendaje?” Joshua aliuliza. Lakini lilikuwa sio swali alilopasa kumuuliza Linda, lakini alifanya hivyo.
Linda hakulipenda swali hilo aliwaza ‘Haoni hali yangu au?’ akaamua tu ajibu “Nimesimama kwa sasa nitarudi nikirejea katika hali yangu”
“Safi… nilidhani umekata tamaa ...niliandaa hotuba nzima ya kukuasa” alisema Joshua kwa utani. Linda alionesha kutabasamu lakini Joshua alikua anamvuta kwenye hoja yake muhimu sana.
“Tuachane na hayo… hebu niambie unaendeleaje Dada Linda?” aliuliza Joshua.
Kichwani kwa Linda maswali yasiyo kuwa na majibu bado yalikuwa yanapita, ‘Anamaanisha nini? Hivi hanioni au? Au anataka nini?’ lakini kwa mara nyingine tena akaamua tu kujibu, “Naumwa sana Kaka Joshua kama unavyoniona”
Joshua alivuta pumzi kisha akaendelea. “Sikia nikwambie kitu Dada yangu, najua unaumwa ila nilichomaanisha unaendeleaje ‘wewe’ sio kimwili bali ‘kiroho’”
Linda alikuwa kama mwenye kushtuka, hakuelewa anamaanisha nini hata kama alimwelewa lakini tena kichwani alijiuliza ‘Nakuaje vizuri kiroho wakati kimwili nimedhofu sana?’ alikaa kimya, hili hakujibu. Kwa vyovyote vile Linda sasa hakuhitaji kufundishwa kuhusu dini alichohitaji ni kupona na kurudi chuoni akamalize masomo yake. Alichoka kusikia kuhusu habari hizo na hakuzisadiki.
“Mama aliniambia mmezunguka makanisa kadhaa kutafuta uponyaji. Sahihi? Aliuliza Joshua. Linda alitikisa kichwa kukubaliana naye. Joshua aliendelea, “Nimekuja kukujulia hali na sio kukuchunguza hali yako ya kiroho. Mimi sio muhubiri wala mchungaji lakini najua hili…. Uponyaji unaanzia ndani ya mtu mwenyewe. Hata mabadiliko, maendeleo yote yanaanza na mtu mwenyewe”
“Unamaanisha nini?” aliuliza Linda.
Joshua alitabasamu kidogo, akamtazama Linda kwa macho yenye huruma. Kisha akasema, "Linda, kuna mstari katika Biblia ambao unanipa nguvu kila ninapopitia changamoto. Unapatikana katika Mithali 4:23, unasema:
'Linda moyo wako kuliko yote uyalindayo; maana ndiko zitokako chemchemi za uzima.'
"Hii ina maana kwamba uzima wako wa kweli, nguvu zako, na uponyaji wako vinaanza na kile kilichoko ndani yako. Unapochagua kulinda na kujaza moyo wako kwa matumaini, imani, na amani, ndipo nguvu ya kweli ya mabadiliko na uponyaji inapoanza kutenda kazi."
Joshua akashika mkono wa Linda kwa upole, "Sijui hali yako kwa undani, lakini najua Mungu anaweza kukuimarisha. Kuwa na amani, na usikate tamaa."
Joshua alitulia kwa sekunde chache, aliona Linda anaingia kwenye tafakari ya kile alichomwambia na maneno yale kweli yalimwingia. Kisha Joshua akaamua kuaga, akasimama taratibu akapiga hatua kuelekea mlangoni. Mama Linda naye akarejea sebuleni:
“Jamani Joshua unaondoka. Kunywa hata chai?” alihimiza Mama Linda.
“Hapana Mama. Ninawahi sehemu, nitakuja siku nyingine”
“Jamani, mwanangu kidgo tu!” alisisitiza Mama Linda lakini Joshua alibaki na msimamo wake.
Aligeuka kwa mara ya mwisho na kusema kwa sauti tulivu lakini yenye msisitizo akimtazama Linda, "Linda, usisahau, uponyaji ni safari ya ndani. Chagua kulinda moyo wako, kwa sababu pale ndipo kila kitu kipya kinaanza."
Linda alimuangalia Joshua akisonga nje, akionekana kama mtu aliyebeba amani isiyoyumba. Mlango ulipofungwa nyuma yake, uliacha sauti ya utulivu, Linda alibaki ameketi kimya, macho yake yakiangazia sehemu isiyojulikana.
Maneno ya Joshua yaliendelea kugonga mawazo yake kama mawimbi yanavyogonga mwamba: "Uponyaji unaanzia ndani ya mtu mwenyewe… Linda moyo wako kuliko yote uyalindayo…" Alihisi kama ujumbe huo ulikuwa mwanga wa tumaini, chachu ya kuanza safari mpya. Alisikia mshindo dhaifu wa gari la Joshua likiondoka, lakini mawazo yake yalikuwa yamezama kwenye tafakari. Aliweka mkono kifuani mwake, akijaribu kuhisi chemchemi ya uzima aliyotajiwa. Kwa mara ya kwanza baada ya muda mrefu, aliwaza, labda bado kuna nafasi ya mabadiliko.
Huo ulikuwa ni mwanzo wa uponyaji wake baada ya kuteseka na kuhisi hakuna msaada. Hakupona ghafla kama alivyotarajia mara ya kwanza, sasa alikuwa amejeaa matumaini na kila siku ilikuwa ni ya tofauti kwake. Kwanza nguvu zake zilirejea kisha maumivu yalipungua na alipotumia dawa alizopewa hospitalini alizidi kuimarika.
Zilipita wiki mbili na sasa alikuwa amerejea kwenye hali yake ya kawaida. Ndani siku hizo chache alifanya mabadiliko kadhaa ya kiroho, alifungua ukurasa mpya. Wakati kwa wakati alitafakari ni nini kilichokuwa kinamsumbua. Alilinganisha kilichompata na hadithi ya Ayubu kwenye Biblia, wakati watu wengi wanajaribu kutafuta jibu la ‘Kwanini watu wema wanataseka?’ Kitabu hicho hakijibu swali hilo bali kinaibua maswali muhimu zaidi ; “Je Mungu ni wa haki? Na Je Mungu anatawala Ulimwengu kwa misingi ya haki?”
Kuna wakati wazazi Linda walifikiri labda amerogwa lakini haikuwa wazi. Au labda kuna kitu Linda alifanya na basi Mungu akamuadhibu: Linda alifikiria hivyo mara kadhaa. Alitamani hadi kufa kuliko kuendelea kuteseka kwa kitu asichokijua chanzo chake.
Ayubu kutoka kwenye Biblia alikuwa mkamilifu na mwelekevu, ni mmoja aliyemcha Mungu na kuepukana na uovu. Hata Mungu alijisifia kupitia yeye lakini Mungu mwenyewe aliruhusu mabaya yamkute. Linda alifikiria zaidi pale Mungu alipomjibu Ayubu alivyomlamikia kuhusu uaminifu na unyenyekevu wake kwake na akaamuru maelezo ya kwanini ameruhusu mabaya hayo yamkute.
Ayubu alijibiwa:Alikuwepo wapi misingi ya nchi ilipowekwa? Au nyota zilipopangwa? Amewahi kuendesha mawio au machweo au hali ya hewa na vipindi vyake? Mungu ana macho yake kwenye vitu vyote hivyo ambavyo hakuna mtu anavifikiria. Vipi kuhusu majira ya wanyama kuzaa, vipi kuhusu uhuru wao, wanyama wa kufugwa na wa mwituni? Ni nani hukazia fikra vitu hivyo.
Mkataa wa linda ulikuwa: tunaishi katika dunia ambayo ni nzuri lakini sio timilifu, maneno ya Mungu ni sheria na ni mazuri lakini pia yanaweza kuwa ni hatari kama mtu asipoyafuata. Swali kwamba ‘Kwanini kuna mateso duniani?’ Mungu amelijibu kuwa tunaishi kwenye dunia ambayo ni nzuri na imeundwa kutozuia mateso lakini zaidi anataka uaminifu, utu na hekima.
Hali yake ilipoimarika zaidi Linda aliamua kurudi chuo ili awahi kufanya mitihani ya mwisho na majaribio kadhaa aliyokosa. Kwasababu alikuwa na ruhusa alikubaliwa lakini changamoto ilikuwa hakujiandaa vizuri na hakuwa na mda wa kutosha kujibu mitihani hiyo vizuri. Alijitahidi kuifanya kwa akili zake zote lakini mitihani kadhaa ilimuangusha akapewa nafasi ya kurudia mwaka. Linda hakuwa tayari kufanya hivyo, dira yake ilikuwa inaangazia mbele tu kwasasa. Kurudia mwaka hakukuwa kwenye mipango yake. Ilimbidi afanye maamuzi magumu lakini sio kurudia mwaka.